Wanafunzi wa shule ya sekondari Sangara wanajengewa ujuzi wa kilimohai na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii (CDTF) walipokuwa wakiandaa na kupanda bustani ya kilimohai iliyopo shuleni katika kata ya Msongola mwezi Agosti 2024.
Mradi wa Maji na Kilimo Hai na Uchumi ni mradi uliobuniwa na wananchi wa Kata ya Msongola kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa na halmashauri ili kuondoa changamoto za uhaba wa maji kwa wananfunzi wanaosoma shule ya sekondari Sangara. Mradi pia unawajengea ujuzi wa kuanzisha na kusimamia bustani ya kilimohai, elimu ya fedha na uchumi wanafunzi na wananchi waishio jirani na shule.
Wanafunzi walipewa elimu kufahamu kilimohai na kutofautisha kati ya kilimo hai na kilimo cha kawaida. Pia jinsi ya kuandaa viwatilifu na mbolea kwa njia za asili, kuandaa shamba, mashimo ya kupandia, na hatua za kupanda mche wa papai kwenye bustani. Wanafunzi walifundishwa kwa nadharia na kwa vitendo kupitia shamba darasa lililopo shuleni.
Lengo la mradi ni kuwaongezea uelewa wa fursa mbalimbali zitakazowasiaida kujiajiri wamalizapo shule, pia bustani kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuendelea kuhudumia miundombinu ya maji iliyowekwa shuleni.
Taasisi ilichimba kisima na kuweka tenki la maji mwaka 2022/2023 lililowezesha upatikanaji wa maji wakati wote shuleni. Maji yanayopatikana yanatumiwa na wananfunzi zaidi ya 600 wanaosoma shuleni, maji ya ziada yakitumika kwa bustani na utunzaji mazingira.